SUA Yazindua Dawati la Jinsia

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimezindua Dawati la Jinsia chuoni hapo ili kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza na kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii hususani kwenye Vyuo Vikuu nchini. 

Dawati hilo limezinduliwa tarehe 10 Oktoba, 2023 Kampasi Kuu ya Edward Moringe na Prof. Samwel Kabote  aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda ambapo amesema atafurahi kuona Dawati hilo likiwa chachu ya kuimarisha maendeleo ya Jinsia katika maeneo yanayozunguka Chuo chao.

SUA Yazindua Dawati la Jinsia

Amesema, kuna mambo yanafanyika hivyo amelitaka Dawati hilo kufanya utafiti na kuyaibua mambo hayo ambayo wao hawana taarifa nayo kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wanaozunguka Kampasi zao zote ili kuimarisha swala zima la maendeleo ya Jinsia kama sehemu ya taaluma inayopaswa kuchapishwa katika machapisho ya aina mbalimbali.

"Kwa vile tunao Wataalamu wa Sosholojia na pia masuala ya Jinsia hapa chuoni  watusaidie kufanya tafiti mbalimbali ili kuweza kuyaibua yale matatizo ambayo yapo" amesema Prof. Kabote.

Kwa upande wake Dkt. Geoffrey Karugila  akimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa amesema wanatambua kuwa kila mtu bila kujali jinsia yake anamchango wa pekee katika maendeleo ya taasisi yao hivyo wanakusudia kujenga Mazingira ambayo yatawezesha wanajumuiya wote wa SUA kufikia uwezo wao kamili wa kiutendaji bila kujali jinsia zao.

"Zoezi hili linahitaji jitihada zetu za pamoja katika kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa za Elimu, ufikiaji wa Rasilimali na Maendeleo ya kila Mwanajumuiya " amesema Dkt. Karugila.

Naye Dkt. Sarah Chiwamba Mratibu wa Dawati la Jinsia SUA amesema Dawati hilo limeanzishwa na kuzinduliwa kwa kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na azma yao ni kuhakikisha kuwa SUA panakuwa mahali salama kwa ajili ya wanafunzi kujifunza na kufikia malengo yao pamoja na wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi.

WhatsApp Image 2023-10-10 at 8.30.00 PM (1)

Dkt. Sarah Chiwamba Mratibu wa Dawati la Jinsia SUA

WhatsApp Image 2023-10-10 at 8.30.00 PM

Share this page